Aibu! Shule ya Msingi Jijini
Dar, Wanafunzi wakaa chini
huku waalimu wakitumia
Khanga kama Majamvi.
Shule ya Msingi Mtambani
iliyoko Kinondoni jijini Dar es
Saalam, haina samani hali
inayosababisha wanafunzi kukaa
chini, wakati walimu
wanalazimika kutandaza khanga
wanazokalia chini ya miti.
“Shule hii ina upungufu wa
madawati, nusu ya wanafunzi
wanakaa chini, hatuna ofisi za
kutosha za walimu wale wasio
na nafasi wanakaa chini ya miti”,
alisema Mwalimu Mkuu
Emmanuel Munisi.
Aliongeza kuwa tatizo hilo
linawalazimisha wengine
kutandika khanga chini ya miti ili
kufanya kazi kwa sababu ya
ukosefu wa meza za kufanyia kazi
na kwamba mvua inaponyesha
wanalazimika kujikusanya pamoja
na wanafunzi madarasani,
alisema Munisi.
Shule ya Mtambani iko taabani
wakati serikali ilipata chenji ya
rada ya shilingi bilioni 43 ambayo
ilielezwa kuwa pamoja na
kununua vitabu mashuleni pia
itawezesha upatikanaji wa
madawati.
Serikali ya Uingereza ilirudisha
fedha hizo kuanzia mwaka jana
na kwamba jukumu la kununua
vifaa hivyo liliachwa kwa Ofisi ya
Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa, ambayo
inasimamia shule za serikali za
msingi na sekondari.
Shule hiyo ina walimu 41 na
wanafunzi 1,830 inakabiliwa na
uhaba wa madawati, viti na
meza za walimu kwa mujibu wa
Munisi. Aliiambia NIPASHE
Jumamosi kuwa mazingira
mabovu ya shule hiyo ni pamoja
na upungufu wa vyoo, ukosefu
wa sakafu madarasani badala
yake madarasa yana mahandaki
na vumbi kila wakati. Akifafanua,
alisema kuwa shule hiyo
ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa na
wanafunzi 77 na ofisi moja
ndongo kwa ajili ya walimu. Hata
hivyo, kwa sasa ina wanafunzi
1,830 wa kike 917, wavulana 913
na walimu 41.
Alisema hakuna maji safi ya
kunywa na wanafunzi wengi
wanakabiliwa na matatizo ya njaa
yanayosababisha kudondoka
mara kwa mara.
Alieleza kuwa wastani wa
kuanguka ni kati ya watoto
watano na zaidi ambao hutibiwa
kwa kuwekewa drip za kuongeza
maji na sukari mwilini.
Madaktari wanasema tatizo ni
ukosefu wa chakula na nguvu
mwilini kwa hiyo
wanapotundikiwa drip wanapona.
Mwenyekiti wa Serikali za Mitaa
Mtambani, Steven Ngonye,
akizungumzia tatizo hilo alisema
litashughulikiwa pamoja na
upatikanaji wa maji na ukarabati
wa shule hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya
Mtambani Maji Safi Sharifu,
alisema serikali inalitambua
tatizo hilo na imetenga bajeti ya
Sh. milioni 108 kwa ajili ya
madawati na ukarabati wa
vyumba vya madarasa na
kwamba hadi sasa madawati 50
yameshapelekwa shuleni hapo.
Akifafanua zaidi alisema kuna
mpango wa kuongeza vyumba
vya madarasa mawili pamoja na
kufikisha maji safi kazi
itakayogharimu Sh. milioni 20.
CHANZO: NIPASHE
0 comments:
Post a Comment