MLINZI wa Simba, Joseph
Owino amefurahishwa
kurejeshwa kwenye kikosi cha
timu hiyo na yupo tayari
kuivaa timu ya JKT Oljoro ya
Arusha kesho. Owino
alitofautiana na Kocha Mkuu,
Zdravko Logarusic kwa kile
ambacho kocha alidai kuwa
mchezaji huyo wa kimataifa
wa Uganda, alikuwa hajitumi
katika mazoezi.
Kutokana na hali hiyo,
aliamua kumpeleka Owino
kufanya mazoezi na timu B
kwa maelekezo maalumu.
Owino ambaye kwa sasa
amerejeshwa kundini baada
ya kuomba msamaha,
alisema atafuata maelekezo
ya kocha kama anavyotaka na
kusisitiza kuwa hatoruhusu
kutokuelewana tena kujirudia.
“Mimi ni kama binadamu
wengine na katika hali ya
kawaida watu hutofautiana na
hivyo nafurahi tumemaliza
tofauti zetu na tutafanya kazi
poa,” alisema Owino jana Dar
es Salaam.
Akizungumzia hali hiyo,
Msemaji wa Klabu ya Simba,
Asha Muhaji alisema ni
utaratibu wa kawaida kwa
kocha kuwarejesha wachezaji
kwenye timu B hasa pale
mchezaji anapotofautiana na
kocha.
“Kwa kiasi fulani naweza
kusema kuwa hakukuwa na
lolote baya kubwa ila ni hali
ya kawaida kwa watu
kutofautiana ila kizuri ni
kwamba wameshamaliza
tofauti zao na kwa sasa kila
kitu sawa,” alisema Muhaji.
Kwa upande wake, Kocha
Logarusic alisema anataka
kuona nidhamu ikichukua
mkondo wake katika klabu
hiyo hasa kwa wachezaji
kujituma na kufuata
maelekezo yake.
Katika mchezo huo wa kesho
kati ya Simba na maafande
hao wa Arusha, utakuwa ni
wa pili kwa kocha huyo katika
ligi na kisha timu itakwenda
Morogoro kuivaa Mtibwa
Sugar, Februari 5, mwaka
huu.
0 comments:
Post a Comment