TANZANIA imeendelea kupata
miradi mikubwa ya
maendeleo ya kimataifa,
ambapo sasa imeibuka kuwa
mshindi kimataifa na
kukubaliwa kuanzisha mradi
mkubwa wa Kanda ya Kati wa
Uchukuzi. Mradi huo
utakaohusisha miundombinu
ya reli, barabara na bandari
unatarajiwa kuanza
kutekelezwa wakati wowote
nchini.
Akizungumza na waandishi wa
habari Dar es Salaam jana,
Waziri wa Uchukuzi, Dk
Harrison Mwakyembe,
alisema mradi huo ulishinda
miradi 51 ya nchi zingine za
Afrika katika mkutano wa
Uchumi wa Dunia (WEF)
uliofanyika Januari 22 jijini
Davos, Uswisi.
Kabla ya ushindi huo, mradi
huo uliingia kwenye miradi 16
bora kati ya 51 ya Afrika na
kushindanishwa katika
mkutano huo uliohudhuriwa
na nchi kubwa kiuchumi,
kampuni za kimataifa na
mashirika makubwa ya fedha
duniani.
“Kwa kweli ilikuwa neema na
furaha kubwa kwa Tanzania
kupewa heshima hii, kwani
miradi mingine 16
iliyowasilishwa katika
mkutano huo nayo ilikuwa na
sifa nzuri, lakini mradi huu
wa Kanda ya Kati ambao
takribani asilimia 95 ya
utekelezwaji wake itanufaisha
Tanzania, ulionekana bora
zaidi,” alisema Dk
Mwakyembe.
Kutokana na ushindi huo, Dk
Mwakyembe alimwomba
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda,
aunde Tume maalumu ya
kitaifa, itakayosimamia na
kushughulikia kikamilifu
utekelezaji wa mradi huo, ili
uwe wa mfano Afrika na
duniani kote.
Sifa zilizochangia mradi huo
kutangazwa mshindi kati ya
miradi bora 16 ya Afrika na
aliyekuwa Waziri Mkuu wa
Uingereza, Gordon Brown, ni
pamoja na mikakati
iliyowekwa na Serikali ya
Tanzania chini ya Mpango wa
Matokeo Makubwa Sasa
(BRN) ya kuendeleza Ukanda
wa Kati wa Uchukuzi.
Nyingine ni dhamira ya dhati
ya Serikali ya Tanzania
iliyoonekana, pamoja na
mfumo iliyojiwekea katika
utekelezaji wa mradi huo
unaolenga kupanua bandari
za Tanzania na kufungua zaidi
milango ya kiuchumi kwa nchi
jirani.
Alipopewa nafasi ya
kuzungumza baada ya mradi
huo kutangazwa kushinda
katika mkutano huo,
Mwakyembe alishukuru
washiriki wa kila pembe ya
dunia, kwa kuiamini Tanzania
na kuelezea mikakati ya
utekelezaji wa mradi huo
ambapo hata hivyo
alibainisha upungufu wa
fedha uliopo.
Alisema baada ya kuelezea
changamoto zilizopo katika
hotuba yake, Brown
alimtaarifu kuwa mwaka huu
viongozi wakuu wa nchi
duniani, watakutana Abuja,
Nigeria, kupokea tathmini ya
utekelezaji wa mradi huo
ambapo pia itafanyika warsha
ya maandalizi ya utekelezaji
wa mradi mwanzoni mwa
Aprili nchini.
“Tuna mpango wa kumwomba
Rais Jakaya Kikwete awe
mgeni rasmi katika ufunguzi
wa warsha hii, ili
tuuthibitishie ulimwengu
utayari wa Tanzania kuleta
mapinduzi katika sekta ya
uchukuzi,” alisisitiza Dk
Mwakyembe.
Aidha, alisema kupitia warsha
hiyo, Tanzania imejipanga
kuionesha dunia kuwa na
mipango mizuri na ndiyo
maana akaombwa Waziri
Mkuu aunde Tume
itakayofanya kazi kwa saa 24
kusimamia utekelezaji wa
mradi huo.
Alisema alipendekeza tume
hiyo ya watu wanane ihusishe
wataalamu kutoka wizara za
Uchukuzi, Ujenzi, Fedha,
Shirika la Reli Tanzania (TRL)
na Ofisi ya Waziri Mkuu.
Mradi huo kwa Tanzania
utagusa Bandari ya Dar es
Salaam, maeneo ya
Mashariki, Magharibi na
Kaskazini mwa nchi na
utahusisha nchi za Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Rwanda na Burundi.
Miradi mingine Mradi huo
mkubwa ni kielelezo kingine
cha heshima ya Tanzania
kimataifa, ambapo mwaka
jana wakati wa ziara ya Rais
wa Marekani nchini, Barrack
Obama, nchi ilipata heshima
nyingine ya kutekeleza mradi
mkubwa wa umeme
unaojulikana kama ‘Power
Africa’, utakaoinufaisha nchi
na kuwa kitovu cha uzalishaji
wa nishati hiyo.
Katika mradi huo
unaowezeshwa na Marekani
kwa kushirikisha Serikali na
sekta binafsi, una lengo la
kuiwezesha nchi kuongeza
kiwango cha uzalishaji
sambamba na kupata umeme
wa uhakika, utakoongeza
ajira. Serikali ya Marekani
ilitoa dola bilioni 7 kusaidia
kupatikana megawati 10,000
za nishati hiyo, huku sekta
binafsi ikitoa dola bilioni 9.
Moja ya kampuni kubwa
zinazohusika na mpango huo
ni General Electric (GE),
ambayo imekuwa mstari wa
mbele kuhakikisha mradi
unaendelea kwa kuahidi kutoa
megawati 5,000 kwa gharama
za kawaida kwa Tanzania na
Ghana.
0 comments:
Post a Comment