ads

Saturday, February 1, 2014

WAUZA NGUO ZA NDANI MITUMBA WAIZIDI UJANJA TBS JIJINI MBEYA

12:03 AM By Unknown No comments

WAFANYABIASHARA wa nguo
za ndani zilizo hafifu maarufu
kama mitumba jijini Mbeya,
jana waliwazidi ujanja
maofisa wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) kwa
kuficha nguo hizo wakati wa
operesheni ya kuzikusanya na
kuwakamata wauzaji.
Wafanyabiashara hao
walioonekana kupewa taarifa
ya nini kitafanyika kabla
walificha nguo hizo hatari kwa
afya za wavaaji na baada ya
kumalizika kwa uparesheni
wakazirejesha sokoni na
kuendelea kuziuza kama
kawaida huku wakijigamba
kuwa Serikali haiwawezi.
Awali maofisa wa TBS
walioambatana na askari wa
Jeshi la Polisi na waandishi
wa habari, waliendesha
operesheni ya kukamata nguo
za ndani hususani chupi,
sidiria na soksi katika masoko
ya Sido na Mwanjelwa lakini
hawakufanikiwa kukamata
hata nguo moja katika
masoko hayo yaliyo maarufu
kwa uuzaji wa nguo za
mitumba ikiwemo zilizokuwa
zikitafutwa.
Ajabu ni kuwa
wafanyabiashara hao
walionesha kuwa na taarifa ya
kufanyika kwa operesheni na
kila kona ya masoko hayo
walisikika wakizungumza kuwa
maofisa wa TBS na polisi
wako katika eneo lao
wakifanya operesheni ya
kukamata nguo hizo.
“Umewaona ndio hao
wamekuja kwa ajili ya
kukamata zile nguo. Lakini
wanatafuta tu ukorofi kama
wanataka kukamata nguo za
mitumba si wakamate tu na
mashati basi.
“Kwa nini watilie mkazo
kwenye nguo za ndani pekee?”
Walisikika wafanyabiashara
katika baadhi ya vibanda vya
masoko hayo mawili wakihoji
hali iliyoonesha kuwa hawana
elimu ya kutosha juu ya
athari za kuvaliwa kwa nguo
hizo.
Mahali pekee walikofanikiwa
maofisa hao ni katika Soko la
Mbalizi ambako walifanikiwa
kumkamata mfanyabiashara
mmoja Lusekelo Adam akiwa
anauza soksi za mtumba na
kumfikisha ofisi ya Kamanda
wa Polisi mkoani Mbeya na
kisha kuteketeza soksi hizo
ambazo muuzaji alisema
zilikuwa na thamani ya Sh
200,000.
Akizungumza mara baada ya
kumalizika kwa operesheni
hiyo Ofisa Viwango na
Mkaguzi wa TBS, Paul
Manyirifa alikiri zoezi hilo
kufanyika kwa
wafanyabiashara walio
wadogo na kusema shirika
linaamini wapo
wafanyabiashara wakubwa
ambao ndio huziingiza kwa
njia za panya na kuwataka
wajisalimishe.
Kwa upande wake
Mwanasheria wa shirika hilo,
Baptista Bitao alisema
adhabu kwa mtu yeyote
anayeuza nguo hizo ni kati ya
Sh milioni 50 hadi 100 lakini
pia Mkurugenzi Mkuu wa
shirika ana mamlaka ya kutoa
adhabu isiyopungua Sh
milioni 20.
Naye Kamanda wa Polisi
mkoani hapa Ahmed Msangi
aliahidi kuendelea kutoa
ushirikiano wa kina kukamata
nguo hizo akisema lengo ni
kuona Watanzania hawawi
watu wa kupokea vitu
vitakavyolisababishia hasara
Taifa lao kwa kuingia
gharama ya kutibu maradhi
yatokanayo na nguo hizo.

0 comments:

Post a Comment