ads

Thursday, February 6, 2014

MABOSI WA MASHIRIKA YA UMMA WAPAANDISHWA KIZIMBANI

12:01 PM By Unknown No comments

MABOSI wa zamani wa mashirika
ya umma, Shirika la Viwango
Tanzania (TBS) na Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL), jana walipanda
kizimbani kujibu mashitaka
yanayowakabili kutokana na
uamuzi waliofanya walipokuwa
wakiongoza mashirika hayo.
Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Joseph
Masikitiko, aliieleza mahakama
kuwa, aliyekuwa Mkurugenzi wa
shirika hilo, Charles Ekelege, alitoa
msamaha wa ada ya utawala kwa
kampuni mbili bila kufuata
taratibu.
Masikitiko alidai hayo wakati
akitoa ushahidi katika kesi ya
matumizi mabaya ya madaraka na
kulisababishia shirika hilo hasara
ya Sh milioni 68, inayomkabili
Ekelege.
Ekelege anadaiwa kusababisha
hasara hiyo baada ya kuondoa ada
ya asilimia 50 ambayo ni sawa na
Sh milioni 68, kwa Kampuni za
Jaffar Mohamed Ali na Quality
Motors bila idhini ya Bodi.
Akiongozwa na Wakili Janeth
Machulya kutoka Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa
(Takukuru), Masikitiko alidai kuwa
anazifahamu kampuni hizo kwa
kuwa zilikuwa zinafanya kazi ya
ukaguzi wa magari kutoka nje kwa
niaba ya TBS.
Alidai katika kipindi cha mwaka
2007 hadi 2009 akiwa Meneja wa
Fedha na Utawala, hajawahi
kupokea wala kushughulikia barua
za maombi ya kuondolewa kwa
ada ya utawala kutoka kampuni
hizo mbili.
Kificho
Aidha alidai hakujua kama
kampuni hizo zilipewa msamaha
wa ada, hadi alipopata ripoti ya
ukaguzi wa hesabu za nje ya
mwaka 2008 hadi 2009, na kusikia
kwenye kikao cha Baraza la
Utendaji ambalo kwa sasa ni Bodi
ya Wakurugenzi, cha Septemba 30
mwaka 2011.
Alidai katika kikao hicho yeye
akiwa mualikwa, walipata taarifa
kuwa Menejimenti ilitoa msamaha
wa ada hiyo bila kupata kibali cha
bodi hiyo, ambapo bodi iliona
walitoa msamaha huo kimakosa
na kuwaonya wasirudie tena.
Alidai taratibu za kuomba
msamaha wa ada ni kuwasilisha
barua kwa Mkurugenzi, kisha iende
kwa Mhasibu Mkuu atakayeandika
dokezo kwa Mkaguzi wa Ndani
ambaye ataangalia kama amekidhi
vigezo vya kusamehewa,
itapelekwa kwa Meneja wa Fedha
kisha Mkurugenzi ataipeleka Bodi
ya Wakurugenzi kwa ajili ya
kuidhinishwa.
Akihojiwa na Wakili Majura Magafu
anayemtetea Ekelege, Masikitiko
alidai kuwa, Bodi haikusema kama
Ekelege alifanya kosa, bali ilisema
Menejimenti ilifanya makosa kwa
kutoa msamaha huo bila kupata
kibali.
Inadaiwa kuwa Machi 28, mwaka
2008 na Agosti 7, mwaka 2009,
Ekelege alitumia madaraka vibaya
na kusamehe ada kampuni mbili
kwa asilimia 50, ambayo ni sawa
na Sh milioni 68 bila idhini ya
Baraza la Utendaji kinyume na
utaratibu wa TBS pia
alilisababishia shirika hilo hasara
ya fedha hizo.
Mataka
Meneja Uendeshaji wa Kampuni ya
Kuhifadhi Magari Yanayodaiwa
Kodi, Bartholomew Kijazi,
ameieleza Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kisutu kuwa wanalidai
Shirika la Ndege Tanzania (ATCL)
Sh milioni 206.4.
Kijazi alidai hayo jana wakati
akitoa ushahidi katika kesi ya
kutumia vibaya madaraka kwa
kutangaza zabuni na ununuzi wa
magari chakavu 26, inayomkabili
Mkurugenzi wa zamani wa shirika
hilo, David Mattaka na wenzake
wawili.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali,
Shedrack Kimaro, Kijazi alidai
kuwa wanaidai ATCL fedha hizo
kutokana na kuhifadhi magari tisa
katika ghala lao lililopo Mbagala,
tangu 1998 hadi Novemba mwaka
jana.
Alidai kuwa Desemba 16, 2011
aliandaa ripoti ya mtiririko wa
kuingiza na kutoa magari 26 ya
kampuni ya ATCL pamoja gharama
za kuhifadhi na kukarabati, baada
ya Taasisi ya Kupambana na
Kuzuia Rushwa (Takukuru) kuomba
ripoti hiyo.
Alidai wakati huo walikuwa
wanaidai ATCL dola za Marekani
118,000 kutokana na kuhifadhi
magari hayo kwa miezi 39 kwenye
ghala lao la Mbagala, ambapo kati
ya magari hayo, magari 15
yalitolewa na mengine tisa
yamebaki kutokana na kukosekana
kwa fedha za kulipa ushuru wa
forodha.
Alifafanua kuwa kwenye ghala lao
wanatoza kila gari dola 250 kwa
mwezi na hadi kufikia Novemba
mwaka jana, walikuwa wakidai
shirika hilo dola za Marekani
129,000 ambayo ni sawa na Sh
milioni 206.4.
Alidai ATCL walihifadhi magari
hayo katika ghala lao kuepuka
gharama za bandarini ambapo kwa
siku wanatoza dola za Marekani 25
hadi 40 kulingana na ukubwa wa
gari na kwa mwezi ingekuwa dola
1,200.
Mbali na Mattaka washitakiwa
wengine ni Kaimu Ofisa Mkuu wa
Kitengo cha Fedha, Elisaph Ikomba
na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Ndani, William Haji.
Washitakiwa wanadaiwa kula
njama, matumizi mabaya ya
madaraka na kuisababishia Serikali
hasara ya dola 143,442.75 za
Marekani kwa kuagiza magari 26
chakavu kwa gharama ya Dola
809,300 kutoka Kampuni ya Bin
Dalmouk Motors ya Dubai bila
kutangaza zabuni ya ushindani.
Aidha wanadaiwa kuruhusu
kununuliwa kwa magari hayo bila
mkataba wa ununuzi ambao
umewekwa saini na wahusika na
kuthibitishwa na Mwanasheria
Mkuu wa Serikali na kuisababishia
Serikali hasara baada ya
kushindwa kulipia kodi na
kuchukua mkopo kwa ajili ya
kuyakomboa na kuyatunza.

0 comments:

Post a Comment