ads

Wednesday, February 5, 2014

WACHINA WALIO KUTWA NA MENO YA TEMBO YENYE THAMANI YA TSH.BILIONI 5.4 WAFANYA JARIBIA LA KUTUO RUSHWA ILI WAACHIWE HURU

1:57 PM By Unknown No comments

RAIA watatu wa China
wanaokabiliwa na kesi ya kukutwa
na meno ya tembo yenye thamani
ya Sh bilioni 5.4, wanadaiwa
kujaribu kutoa rushwa ya Sh
milioni 30.2 kwa askari ili
wasifunguliwe mashitaka.
Wakili Mwandamizi wa Serikali,
Faraja Nchimbi alidai hayo jana
katika Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu wakati akiwasomea
washitakiwa maelezo ya awali.
Alidai Novemba 2 mwaka jana
katika eneo la Kifaru Mikocheni B,
washitakiwa walikamatwa na
askari wakiwa na vipande 706 vya
meno ya tembo pamoja na ganda
la risasi.
Nchimbi alidai washitakiwa hao,
walikiri kumiliki vitu hivyo bila
kibali na kudai watawapa askari
hao na baadhi ya wananchi
waliokuwa katika eneo la tukio Sh
milioni 30.2 ili wasifunguliwe
mashitaka.
Hata hivyo, askari hao, Mrakibu
wa Polisi (ASP) Heri Mugaye,
Sajenti Gerwin, askari wa
Wanyamapori Simon Saye na
wananchi waliokuwa eneo la tukio,
walikataa kupokea fedha hizo na
kuwafikisha kituo cha Polisi na
kuwafungulia mashitaka.
Aliendelea kudai kuwa katika
maelezo ya onyo waliyotoa kituo
cha Polisi, washitakiwa hao walikiri
kukutwa na nyara hizo na risasi
bila kuwa na kibali cha umiliki
kutoka mamlaka husika.
Hata hivyo, jana baada ya
kusomewa maelezo ya awali,
washitakiwa hao waliokuwa
wanatafsiriwa na mkalimani,
walikana maelezo hayo, lakini
walikiri majina, uraia na umri wao.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni
Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na
Chen Jinzhan (31), walifikishwa
mahakamani hapo Novemba 8
mwaka jana, wakikabiliwa na
shitaka moja, kabla ya kuongezewa
mashitaka mawili.
Awali, Wakili Mwandamizi wa
Serikali, Tumaini Kweka,
aliwasomea upya washitakiwa
mashitaka yao baada ya kufanya
marekebisho kwa kuongeza
mashitaka mawili .
Alidai kuwa Novemba 2, mwaka
jana katika mtaa wa Kifaru
Mikocheni B, washitakiwa
walikamatwa wakiwa na vipande
706 vya meno ya tembo vyenye
uzito wa kilo 1,889 vyote vikiwa na
thamani hiyo, mali ya Serikali ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
bila kuwa na kibali cha Mkurugenzi
wa Wanyamapori.
Alidai katika mashitaka mengine,
wanadaiwa kutaka kutoa rushwa
ya Sh milioni 30.2 kwa askari Polisi
na askari wa Wanyamapori ili
wasifunguliwe mashitaka ya
kukutwa na nyara na ganda la
risasi bila kuwa na kibali.
Katika mashitaka mengine,
washitakiwa wanadaiwa siku hiyo
hiyo walikutwa na ganda la risasi
bila kuwa na kibali cha kumiliki
silaha. Washitakiwa hao walikana
mashitaka yao na kurudishwa
rumande hadi Februari 17 mwaka
huu kesi hiyo itakapotajwa tena.

0 comments:

Post a Comment