ads

Wednesday, February 5, 2014

VIJANA WAHIMIZWA KUJISHUGHULISHA NA KILIMO MKOANI MBEYA

2:06 PM By Unknown , No comments

SEKTA za elimu na kilimo ni
miongoni mwa zile zilizoingizwa
katika mpango wa Matokeo
Makubwa Sasa (BRN).
Lengo la serikali katika mpango
huo ni kuona sekta lengwa
zinapiga hatua za haraka na kuwa
na tija kwa watanzania. Ni kwa
kutambua umuhimu wa mpango
huo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,
Abbas Kandoro aliamua kufanya
ziara ya siku tatu wilayani Mbozi ili
kuona maandalizi ya utekelezaji wa
mpango wilayani hapo.
Dhana iliyopo ni kwamba mpango
huo, BRN, hauwezi kufanikiwa
iwapo hakutakuwa na maandalizi
stahiki ambayo pia kama ulivyo
mkakati wenyewe lazima nayo
yafanyika kwa haraka zaidi
sambamba na usimamizi mzuri wa
mpango mzima. Akiwa wilayani
hapa, Kandoro alijikita zaidi katika
sekta mbili hizo, elimu na kilimo
ambazo ni nguzo muhimu katika
suala zima la maendeleo kwa
wananchi wa wilaya hii.
Ukaguzi wa miundombinu ya
kilimo hususani maghala ya
chakula, matumizi sahihi ya pesa
zinazotolewa na serikali pamoja na
maabara mashuleni ni miongoni
mwa mambo aliyoyazingatia
kwenye ziara yake.
Kujiunga katika vikundi
Kandoro aliwahimiza wakulima
wilayani hapa kujiunga katika
vyama vya ushirika kwa kuwa ni
muhimu katika kuwasaidia kupiga
hatua kimaendeleo.Kwamba mbali
na ukweli kuwa umoja na nguvu,
vikundi vya ushirika vinakopesheka
kirahisi tofauti na mtu anapokuwa
mmoja mmoja.
Aliwataka wakulima kutokatishwa
tamaa na kasoro za viongozi
wachache wanaokwamisha vikundi
vyao au vyama vya ushirika
kushindwa kufikia malengo ya
kuwasaidia wanachama wake.
Alisema jambo muhimu kwa
wakulima ni kutambua kuwa
vyama vya ushirika pia vinaweza
kuwatetea hata katika kupata
maslahi stahiki kwa kuuza mazao
yao. Kupitia vyama vya ushirika,
Kandoro alisema serikali mkoani
hapa imelenga kuhakikisha mfumo
wa stakabadhi ghalani unatumika
na kuwawezesha wakulima
kuondokana na kutapeliwa na
wafanyabiashara wanaokwenda
kuwalaghai majumbani wakiwataka
kuwauzia mazao kwa bei rahisi.
Akizungumza na wanachama wa
kikundi cha wakulima wa kahawa
cha Iganda kilichopo kijijini Isansa,
Kandoro alisisitiza msimamo wa
serikali ya mkoa kuona kwamba
mkulima hauzi kahawa mbichi
badala yake aikaushe mwenyewe.
“Stakabadhi ghalani inaambatana
na uwepo wa maghala.
Ndiyo sababu tumenuia kukarabati
jumla ya maghala 54 kwa wilaya
yote ya Mbozi na kwa kuanza
tutakarabati kwanza maghala 24.
“Tunataka msimu wa kuvuna
kahawa unapoanza mfumo huu
uwe umeanza kufanya kazi. Kwa
maana hiyo kahawa itakayovunwa
itakusanywa kwa mfumo huo na
kuhifadhiwa katika maghala
haya.“Tunataka wakulima wawe na
sauti itakayowawezesha kunufaika
na jasho lao,” alisisitiza.
Mkuu huyo wa mkoa amesema
ataangalia uwezekano wa
kukisaidia kikundi hicho kupata
mashine kubwa ya kukoboa
kahawa kwa kuwa iliyopo hivi sasa
ina uwezo mdogo wa kufanya kazi,
hali inayosababisha baadhi ya
wakulima kwenda kwingineko
kukoboa kahawa yao.
Vijana na kilimo
Katika ziara hiyo, Kandoro
aliwapongeza wakazi Mbozi kwa
kuendelea kujituma katika kilimo
huku akisema kwamba ni lazima
jamii ikubali kuwa kilimo kitabaki
kuwa ajira kubwa ya watanzania
na hivyo kinachotakiwa ni serikali
kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali kuzidi kuboresha
miundombinu yake.
Mkuu huyo wa mkoa anaamini
kwamba miundombinu ikiwa bora
wakulima nao watafanya shughuli
zao kwa urahisi zaidi. “Na vijana
wanapaswa watambue kuwa si
kweli mijini kuna maisha bora.
Wengi wanadanganyika kukimbilia
huko na kuacha ajira hii.
Wanakwenda kuishi maisha
magumu mijini na kuishia
kujiingiza kwenye biashara zisizo
na tija wakati wangeweza kujiajiri
vijijini kwao kwa kulima mazao
kibiashara,” alisema.
Alisema ni vyema sasa jamii ikawa
na mtazamo kuwa vijana
wanaweza kunufaika na kilimo
wakiamua na kuwa serikali ya
mkoa itazidi kuandaa mikakati
mbalimbali ya kufanya kilimo kiwe
na tija.
“Nawapongeza kwa kuona mnazidi
kujituma. Mazao yanastawi vizuri
hali inayoonesha kwamba
mmetumia utaalamu. Tutazidi
kuleta wataalamu kila
inapowezekana ili waweze
kusaidiana nanyi,” alisema.
Kujaribu mazao mengine
Katika kijiji cha Senjele, mkuu
huyo wa mkoa alibaini kuwa ardhi
na hali ya hewa ya ukanda wa juu
wa wilaya ya Mbozi usiokubali
kilimo cha kahawa unaweza
kustawisha zao la korosho.
Hii ilikuja baada ya kushuhudia
miti ya korosho ikiwa imestawi
vyema katika viunga vya Shule ya
Sekondari ya Shikula.
“Halmashauri kwa kushirikiana na
ofisi ya kilimo mkoa angalieni
namna mnavyoweza kuhimiza
kilimo cha korosho katika ukanda
huu. Hawa hawajapanda kama
urembo hapa.Wasaidieni pia dawa
ya kupulizia hawa waliokwisha
anza. Ni zao linaloweza kuinua
uchumi wa Wanambozi
tukilihamasisha kulimwa,”
anasema.
Ufisadi na kutowajibika
Hata hivyo, Kandoro aliweza
kubaini kasoro kadhaa zinazoweza
kukwamisha matokeo ya haraka
katika sekta ya kilimo wilayani
Mbozi. Kasoro hizo ni matumizi
mabovu ya fedha za serikali katika
utekelezaji wa miradi ya
miundombinu ya kilimo pamoja na
baadhi ya wataalamu kutowajibika
ipasavyo.
Moja ya maeneo yaliyobainika
kuwepo na ufujaji wa fedha za
serikali ni katika mradi wa
umwagiliaji wa Iyula B uliopo
katika kata ya Iyula. Hapa Kandoro
alibaini kuwepo na upotevu wa
fedha kiasi cha zaidi ya Sh milioni
115.
Awali katika taarifa iliyosomwa na
ofisa kilimo na mifugo wa kata ya
Iyula, Khalid Mchomvu
alibainishwa kuwa ujenzi wa banio
la maji la mradi huo umegharimu
kiasi cha Sh 255,710,000 na
unatarajia kunufaisha jumla ya
kaya 268 zitakazolima ekari 210 za
kilimo cha umwagiliaji zikiwemo
ekari mbili zilizotengwa kwa ajili ya
vijana.
Kilichomkera mkuu wa mkoa ni
baada ya Ofisa Kilimo na Mifugo
wa Halmashauri ya Wilaya, Richard
Siliri, kueleza kuwa zinahitajika
fedha nyingine kwa ajili ya
kupasua kwa baruti jiwe kubwa
linalozuia maji kupita kwenye
mfereji pamoja na kuusakafia
mfereji huo wenye urefu wa
kilometa tisa.
Hapo ndipo mkuu wa mkoa
aliposema hakuna sababu ya
mradi huo kuombewa fedha
nyingine wakati hesabu za
kiukaguzi zinabainisha kuwa kutoka
mfuko wa maendeleo ya kilimo wa
wilaya (DADPs) walikwisha pewa
zaidi ya Sh milioni 250 na
walizotumia hadi mradi ulipofikia
ambapo ujenzi wa banio
umekamilika ni Sh milioni 134.
Fedha hizo walipewa kwa awamu
mbili ambapo awamu ya kwanza
walipewa zaidi ya Sh milioni 115
na ya pili wakapewa zaidi ya Sh
milioni 134. Akahoji ni kwa nini
taarifa ya ukaguzi inayobainisha
matumizi ya Sh milioni 134 hadi
mradi huo ulipofikia zinatofautiana
na taarifa za watendaji hao.
Akasema kuna uwezekano mkubwa
kuwa fedha hizo zilitafunwa na
wachache kwa manufaa yao.
“Nasema fedha mnazo kwa mujibu
wa taarifa za ukaguzi. Mnaweza
kukamilisha ujenzi wa mfereji na
zikabaki. Mliomba jumla ya Sh
milioni 340 kwa ajili ya utekelezaji
wa mradi na tayari mmepewa zaidi
ya Sh milioni 250 na mmetumia Sh
milioni 134 hizi nyingine ziko
wapi?” Akahoji.
Akaendelea: “Nawahakikishia
ndugu zangu wananchi kuwa
tutashirikiana kuhakikisha fedha
zenu zinajulikana zilikokwenda.
Hatuwezi kukubali miradi ya
serikali kukwama kutokana na
wajanja wachache kujinufaisha.”
Akizungumza na waandishi wa
habari, mwenyekiti wa kamati ya
usimamizi wa mradi huo, Jua
Mwamlima, alisema fedha za
mradi zilizokwishatolewa kwenye
akaunti ni zaidi ya Sh milioni 250
na zilizosalia kwenye akaunti hiyo
ni Sh 500,000 pekee.
Akasema wanachojua wanakamati
ni kuwa fedha zote zilitumika
kwenye mradi hadi ulipofikia hivi
sasa kwa kuwa nyaraka zote za
malipo zilikuwa zikiandaliwa na
kufanywa na maofisa wa ngazi ya
juu na wao kupelekewa kwa ajili ya
kutia saini pekee. Ubadhirifu
mwingine ukabainika katika kijiji
cha Msiha.
Sh milioni 100 zilizotolewa na
serikali kwa ajili ya ujenzi wa
bwawa la maji ya kutumia
majumbani pamoja na kilimo cha
umwagiliaji katika kijiji hicho
haijulikani zilipo. Kufika kwa
Kandoro kijijini hapo kulilenga
kuona namna miundombinu ya
bwawa hilo ilivyojengwa akijua
kwamba lilikwishafikia hatua nzuri
tayari kuanza kuwanufaisha
wananchi walengwa wanaokabiliwa
na uhaba wa maji kwa ajili ya
matumizi ya majumbani na pia
kwa ajili ya kilimo.
Baada ya kufika na kukuta hakuna
lolote lililofanyika ndipo mkuu
huyo wa mkoa aligeuka mbogo na
kutaka ofisi ya kilimo imueleze
ilimpeleka hapo kufanya nini
wakati hakuna miundombinu na
pia akataka kujua fedha zote
walizopewa zilifanya kazi gani.
“Sasa hapa naomba mnieleze
mmenileta kufanya nini?
Mimi nilijua kuna miundombinu
iliyokwishajengwa tayari kwani ni
muda mrefu tangu mmepewa
fedha. Je, mlinileta kuja kushangaa
mandhari ya pori hili na kusimama
simama tu kama hivi?” akahoji.
Kwa mujibu wa Kandoro, ofisi ya
kilimo wilayani hapo katika mwaka
wa fedha 2010/2011 ilipewa kiasi
cha Sh milioni 40, na mwaka wa
fedha 2012/2013 ikapewa kiasi cha
Sh milioni 60 lakini fedha hizo
hazijulikani ziliko na hakuna kazi
yoyote iliyoanza kufanyika mpaka
anafika eneo la mradi.
“Mimi nilitaraji leo nakuja kuona
miundombinu iliyolenga kusaidia
kuweka mtiririko mzuri wa maji ili
maji hayo yasaidie kulima kwa
uhakika. Hakuna kitu hapa! Wewe
mwenyewe hauna uhakika na
kilichoendelea katika Sh milioni
100 zote zilizoletwa,” akasema
Kandoro akimwambia Ofisa kilimo
na mifugo wa wilaya ya Mbozi,
Richard Sirili.
“Hii haikubaliki hata kidogo na
nasema lazima tuchukue hatua
hata polisi watu watapelekwa.
Nimeshtuka pesa ni nyingi mno.
Serikali inaleta pesa hakuna
kinachofanyika. Hatuwezi kwenda
kwa mwendo huu ndugu zangu,”
alisisitiza.
Mmoja wa wakazi wa kijiji cha
Msiha, Mawazo Mwamlenga
alisema bwawa hilo linasubiriwa
kwa hamu kubwa na wakazi wa
kijiji hicho kutokana na kukabiliana
na uhaba mkubwa wa maji kwa
ajili ya matumizi ya majumbani na
kuendeshea kilimo cha
umwagiliaji, alichosema kitaweza
kuwakomboa kuondokana na
umasikini.
Kuendelea kusuasua kwa ujenzi wa
bwawa hilo ilhali wakazi wanayo
taarifa kuwa serikali ilikwishatoa
fedha kunaonesha kama kwamba
wakazi hao wametumika kama
mtaji wa kunufaisha wajanja
wachache wasio na huruma kwao.
Katika kata ya Myovizi, Kandoro
alikutana pia na malalamiko
yanayokwamisha maendeleo ya
kilimo.
Kubwa ni mtaalamu wa kilimo
kulalamikiwa kwa kutowajibika
ipasavyo kwa wananchi aliopewa
jukumu la kuwatumikia kutokana
na utaalamu wake. Ofisa huyo,
Rehema Mwandurusa, mbali na
kudaiwa kuishi mbali na kituo
chake cha kazi wakazi wa kijiji cha
Ichesa katika kata hiyo wanasema
wamekuwa wakiishi kama hawana
mtaalamu wa kilimo hivyo
kulazimika kuendesha shughuli zao
pasipo utaalamu wowote.
Mwenyekiti wa halmashauri wa
wilaya ya Mbozi, Eliki Ambakisye
pia akakiri ofisa huyo kukaidi agizo
la kumtaka aishi eneo lake la kazi
na badala yake amekuwa akiishi
katika mji mdogo wa Mlowo uliopo
takribani kilomita kumi kutoka
eneo hilo. Akasema kwa kuishi
mbali na eneo la kazi ofisa huyo
amekuwa akifika kwa kusuasua
sana katika eneo hilo, hivyo uwepo
wake hauwasaidii wananchi
aliopewa dhamana ya
kuwatumikia.
Kufuatia malalamiko hayo,
Kandoro akamuagiza ofisa huyo
kuchagua jambo moja kati ya kazi
na kuishi anakotaka yeye ili nafasi
yake apewe mtu aliye na utayari
wa kuishi katika eneo lake la kazi
ili kuwatumikia wananchi.
Uhaba kidato cha sita
Upande wa sekta ya elimu nao
ulikuwa na yake. Cha kwanza
kilichojitokeza ni uhaba wa shule
za sekondari kwa ajili ya elimu ya
kidato cha tano na sita.Katika
eneo hilo, Kandoro alifurahishwa
na uamuzi wa wakazi wa kata ya
Myovizi kuongeza vyumba vya
madarasa na kujenga mabweni
kwa ajili ya kidato cha tano na
sita. Mkuu huyo wa mkoa aliahidi
kuchangia Sh 500,000 kwa ajili ya
ujenzi wa vyumba vya madarasa
unaoendelea.
Mkuu huyo wa mkoa aliwataka pia
wanafunzi wanaosoma michepuo
ya sayansi katika shule zilizo
wilayani hapo kutambua kuwa
wanalo jukumu la kuikomboa nchi
kuondokana na changamoto ya
uhaba wa walimu wa masomo ya
sayansi. Akaziagiza halmashauri
kuziwezesha shule zilizo na
maabara kwa kuzifungia umeme
wa mionzi ya jua ili kutoa fursa
kwa wanafunzi kujifunzwa kwa
vitendo wakati wowote.
Mimba mashuleni
Lakini suala la mimba kwa
wanafunzi likaonekana kuwa ni
changamoto nyingine inayopaswa
kuendelea kutafutiwa ufumbuzi.
Mkuu wa mkoa aliagiza hatua za
kisheria kuchukuliwa dhidi ya
wahusika wa mimba za wanafunzi,
ikiwa ni pamoja na kuwawajibisha
wazazi wanaokwamisha kesi za
mimba kutofanyika kisheria.
Ni katika kulipa uzito jambo hili
alitoa muda wa siku saba kwa
ofisa mtendaji wa kata ya Nanyala,
Theofrida Hankungwe kuhakikisha
amewasilisha taarifa za hatua
zilizochukuliwa kwa wanafunzi
watano wa kike waliopata mimba
mwaka 2013 katika Shule ya
Sekondari ya Shikula.
Agizo hilo pia lilitolewa kwa mkuu
wa shule hiyo, Chonge Dafa
ambapo kwa pamoja viongozi hao
wanapaswa kueleza ni hatua zipi
zilichukuliwa kwa wanafunzi
waliopata mimba na pia
waliosababisha. Wanafunzi hao ni
pamoja na mmoja aliyepewa
mimba na mwanafunzi mwenzake
ambapo wote walifukuzwa shule.
“Kumekuwa na mchezo wa baadhi
ya wazazi kumaliza kesi za mimba
kiundugu kwa kupeana pesa au
mali nyingine badala ya kupeleka
kesi hizo mahali husika ili hatua za
kisheria ziweze kuchukuliwa.
Matokeo ya kumalizwa kwa kesi
hizo kienyeji imekuwa ni kuendelea
kwa wimbi la mimba mashuleni na
kusababisha watoto wa kike
kukosa haki yao ya msingi ya
kupata elimu.
“Ndugu zangu lazima tukubali
kuwa ukimwelimisha mtoto wa
kike umeelimisha familia yake
yote. Sisi akina baba mara nyingi
hatukai na watoto nyumbani. Ni
akina mama wanaoshinda nao na
kuwapa malezi ya karibu sasa
kama mama akiwa na elimu ni
wazi atailea familia yake katika
mazingira bora zaidi,” alisema.

0 comments:

Post a Comment